NI APRILI 7 mwaka 2012 tasnia ya filamu ilipatwa na majonzi makubwa kutokana na kifo cha aliyekuwa mwigizaji nguli, Steven Kanumba, ambaye alikuwa kipenzi cha wengi ndani na nje ya nchi.
Licha ya wengi kutokuamini kwa muda huo, baada ya muda ikagundulika kweli amefariki, hivyo majonzi zaidi yakarindima, huku kila mtu akisema lake kuhusu kifo hicho.
Baada ya mazishi yake mashabiki walijipa matumaini kwamba tasnia hiyo licha ya kumpoteza mwigizaji huyo ingeendelea vema kutokana na kuwa na idadi kubwa ya waigizaji wenye sifa kama za Kanumba, lakini hadi leo mwaka wa tatu tasnia hiyo inaonekana kupoteza mvuto.
Mwigizaji, Yobnesh Yussuf ‘Batuli’, alipotembelea Kampuni ya New Habari (2006) Ltd , aliongeza chachu ya kutaka kujua zaidi anamkumbukaje Kanumba ambaye waliwahi kufanya kazi kwa ukaribu.
“Wasanii wengi hatujui tatizo ni nini, ndiyo maana naweza kusema kama ameacha laana kwa kuwa tumekutana mara kwa mara kuzungumzia jambo hilo, lakini kama tumeshindwa tumejitahidi na hakuna aliyeweza kufikia mvuto na uwezo wake kwa mashabiki, ndiyo maana tunaonekana kama tunapoteza mwelekeo na kifo chake ni kama kimeacha laana kwa filamu za Tanzania,’’ anaeleza Batuli.
Batuli, mwenye watoto wawili ambaye amezaa mapema kwa hofu ya uzuri wake kuisha kabla ya kupata motto, anasema wakati mwingine wanajikuta wakisema kwamba kwa sasa wanasubiri muujiza ya Mungu ndiyo kutokee mapinduzi mapya katika filamu za bongo, maana kwa sasa hali imeyumba.
JE Tatizo nini?
Batuli anasema zipo changamoto nyingi zinazowafanya wasifikie mafanikio aliyokuwa nayo Kanumba katika filamu, likiwemo la kutokuaminiwa na wafadhili kunakotokana na baadhi ya waigizaji maarufu wenye majina makubwa katika tasnia hiyo kudhulumu wafadhili hao kiasi kwamba hawataki kufanya kazi na waigizaji wengine wa filamu.
“Wapo wafadhili wameshatoa fedha nyingi kwa baadhi ya masupastaa wetu ili watengeneze filamu zenye ubora na kiwango cha juu ili kuleta hamasa katika soko la filamu kama ilivyokuwa enzi za Kanumba, lakini hakuna aliyethubutu hadi leo, wengi wao wametumia kwa maslahi ya pombe, mapenzi na mambo mengine, wamesahau kwamba walipewa fedha kwa ajili ya kufanyia mapinduzi ya filamu,’’ anaeleza.
Licha ya hayo, Batuli bado anaamini kwamba Kanumba alikuwa na vitu vingi vya ziada vilivyomfanya apendwe ndani na nje ya nchi, vikiwemo uthubutu wake, kujitambua na kuwa na uchungu wa mafanikio.
“Kanumba alikuwa hakurupuki, alikuwa hakati tamaa, hata alipokuwa akichekwa aliamini ipo siku atapigiwa vigelegele, alikuwa mbunifu na mpenda kukosolewa asiye na woga wa kufanya lolote analoona ni fursa kwake,’’ anaendelea kumuelezea.
0 comments:
Post a Comment