+10 344 123 64 77

Thursday, June 18, 2015

IN BONGO!!!! WAKONGWE KATIKA MOVE!!!! FANYENI KITU KUOKOA FILAM ZETU BONGO!!!===>>BOFYA KUJUA MIKAKATI YAO

Wako Wapi Wakongwe Kunusuru Tasnia ya Filamu?
UKIMUULIZA msanii wa filamu wa hapa nchini, kama sanaa hiyo inalipa, atakujibu ndio inalipa. Ukibadili swali hilo na kumuuliza matatizo ambayo anakumbana nayo katika sanaa hiyo kila mara, atakwambia wizi wa kazi za wasanii kwa baaadhi ya watu wachache ambao hupenda kufaidika kupitia migongo ya wasanii hao.
Hayo ndio mambo ya haraka haraka ambayo wasanii wengi wameyatambua katika sanaa hiyo ambayo kila kukicha inapata wasanii chipukizi ambapo kuna baadhi yao hufikiri kuwa tasnia ya uigizaji ni rahisi kwa mtu yeyote yule. Tanzania kama ilivyo katika nchi nyingine, ina vipaji katika tasnia ya filamu, ndio maana kila kukicha wanaibuka wasanii chipukizi ambapo baadhi yao wamekuwa wakifanya vizuri. Kuna badhi ya vikundi vya uigizaji viliwahi kuwepo wakati fulani halafu vikapotea ghafla.
Huenda viliona tasnia hii hailipi na ndio maana vikaamua kusambaratika. Lakini sasa baadhi yake sasa vimeanza kujiunda upya. Huenda vimegundua kuwa Sanaa hiyo kwa sasa inalipa. Kuna vikundi kama vile Mambo Hayo, Kaole na vinginevyo ambavyo vilishawahi kuweka historia ya michezo ya kuigiza na baadae vikazima ghafla.
Siku za hivi karibuni kulikuwa na aina fulani ya mvutano ambao haukuwa rasmi ambapo waigizaji wakongwe walikuwa wakiwaponda wale wa sasa, yaani chipikuzi ambao wamejizolea umaarufu ghafla kuwa wanaingia katika sanaa kwa ajili ya kutafuta umaarufu na si kwa ajili ya kufanya sanaa kama inavyotakiwa.
Kadhalika, kukawa na aina nyingine ya mpasuko ambapo wasanii wa sasa wakawa wanaonekana maarufu kwa kutawala magazeti kila siku kwa visa na mikasa ambayo kwa hali ya kawaida havikutakiwa kuwepo katika magazeti, kwa sababu ya kutokuwa na maana katika jamii iliyowazunguka zaidi ya kutafuta umarufu kama ilivyotafsriwa hapo awali. Mzee Majuto, mwigizaji maarufu aliwahi kusema kuwa tasnia ya filamu imeingiliwa na baadhi ya vijana wachache ambao hawajui maana yake.
Huenda ikawa mtizamo wake, lakini pia kukawa na ukweli ndani yake kutokana na uzoefu alionao mwigizaji huyo ambaye ameshiriki katika filamu mbalimbali hapa nchini na kujipatia umaarufu kutokana na kipaji na uwezo alionao katika kufikisha ujumbe kupitia tasnia hiyo. Alisema kuwa wanataka mafanikio ya haraka haraka pasipo na mipango ya muda mrefu, akamalizia kusema kuwa matokeo yake wanajikuta wakati mwingine wakidhulumiwa kwa sababu ya tamaa.
Mbali na mtizamo wa Mzee Mjuto, kuna wadau wengi ambao wameigawa tasnia hii ya filamu katika makundi mawili, kwa maana ya vijana wa siku hizi ambao wanaitwa wavamizi wa fani na wale wakongwe ambao wameamua kuungana na vijana wachache na kufanya filamu zinazoeleweka. Filamu nyingi za kisasa zimeshindwa kuzingatia maadili; hali kadhalika kuwa na mtiririko mzuri wa ujumbe unaoeleweka.
Kuna baadhi ya filamu, huwezi kujua waigizaji walitaka kufikisha ujumbe gani katika jamii inayowazunguka. Kuna haja ya wasanii wakongwe katika tasnia hii ya filamu kurejea katika ‘fani yao’ ili kuhakikisha inapewa heshima kuliko kuwaachia wachache ambao wanaonekana kama wavamizi kwa kutokuwa na jipya. Hivi karibuni nilisikia kundi la Kaole linarejea, hili ni mmojawapo wa vikundi ambavyo viliwahi kufanya vizuri kabla ya kukaa pembeni kwa muda.
Lakini pia makundi kama vile Mambo Hayo na mengine hayanabudi kurejea. Faida mojawapo ya vikundi hivi endapo vitaamua kurejea kasi ni kwamba Watanzania watapata fursa ya kuangalia filamu zenye maudhui ya Mtanzania na si kuiga kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wa sasa. Tatizo kubwa kwa wasanii wanaoibuka ni kushindwa kuumiza kichwa ili kufahamu hasa ni nini jamii ya Watanzania inahitaji.
Zaidi ya hapo kuna wale ambao wameamua kuangalia filamu za nje na kuzibadilisha kidogo sana huku zikionekana dhahiri kuwa zimetengenezwa katika mazingira ambayo si ya Kitanzania. Kuna umuhimu kwa wasanii wakongwe wa filamu kutolifumbia macho tatizo hilo ambalo linasababisha mmomonyoko wa maadili.
Kuna aina fulani ya kuiga lakini si kuiga kila kitu. Waswahili wanasema akili ya kuambiwa changanya na ya kwako ili upate kitu kamili. Wadau wa soko la filamu pia wanahitaji kuwa na viwango maalumu ambavyo vitazingatia maadili na weledi katika tasnia hiyo. Wasanii wengi wameegemea Nigeria kwa sasa, kwa sababu wamegundua kuwa filamu zao zina soko hapa nchini. Kwa nini wasitengeneze za kwetu pia zikawa bora na zikapata soko huko Nigeria?

0 comments:

Post a Comment