MADEREVA wa bodaboda ambao majina yao hayakuweza kupatikana mara moja, wamenaswa wakizichapa kavukavu baada ya mwenzao kuwazidi fedha za malipo yaliyotolewa na abiria wao.
Tukio hilo la aina yake lilitokea juzikati majira ya saa 7 mchana maeneo ya stendi wilayani Misungwi mkoani Mwanza ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, bodaboda hao (wawili) walidai mwenzao aliwazunguka kwa kuchukua pesa zaidi kutoka kwa abiria waliokuwa wamewabeba na kuwapa pesa kidogo ambayo haikulingani na umbali waliotembea kuwapeleka abiria hao.
Awali, bodaboda wote (watatu) walikuwa katika harakati zao za kusaka abiria ambapo mmoja wao (anayedaiwa kuwazunguka wenzake) alipata abiria watatu waliokuwa wakienda sehemu moja ambao alielewana nao bei ya shilingi elfu mbili (2,000) kwa kila mmoja wao kutoka eneo walipo mpaka eneo walilokuwa wakienda, bei ambayo abiria hao waliiafiki na kumkabidhi pesa hizo ambazo jumla yake ilikuwa shilingi elfu sita (6,000) kisha walimwambia atafute wenzake wawili, akakubali na kufanya hivyo.
Baada ya kuwapata wenzake, bodaboda huyo aliwaongopea kuwa wateja hao wametoa shilingi elfu moja (1,000) kila mmoja hivyo amepokea jumla ya shilingi elfu tatu (3000) kwa madai walikuwa hawaendi mbali.
“Wenzie walikubali lakini wakashangaa safari ni ndefu tofauti na fedha waliyoitoa. Baada ya kuwashusha abiria, walimbana mwenzao, akasema amepewa shilingi elfu moja kwa kila mtu.
“Jamaa hawakukubali, ikabidi wawafuate wale abiria baada ya kuwauliza wakawaambia walimpa shilingi 6000 ndipo walirudi kijiweni na kumkwida mwenzao ambapo naye hakukubali akaanza kujibu mashambulizi hali iliyosababisha timbwili zito,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, bodaboda wenye busara waliingilia kati na kuwataka waache ugomvi, wakae chini kisha waelewane kistaarabu ili wafikie mwafaka ambapo baada maneno hayo walimgeukia bodaboda (anayedaiwa kuwazunguka wenzake) wakamtaka aache tamaa, awape haki yao, ushauri ambao aliuafiki na kurudisha pesa hizo.
0 comments:
Post a Comment