“Naombeni mnisaidie Watanzania wenzangu nateseka mwaka wa nane huu na sina msaada wowote, nimevumilia lakini naona nazidi kuumia bila kupata tiba yoyote, ni bora ningerudi kwetu kama kufa nikafie huko.”
Hivi ndivyo alivyoanza kusimulia mama aliyejulikana kwa jina la Paulina Omary, (58), mkazi wa Ukerewe mkoani Mwanza ambaye sasa hivi yuko jijini Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu wiki iliyopita.
MWANZO WA TATIZO
“Nina miaka nane tangu nianze kuugua ugonjwa huu, ulianza kama uvimbe mdogo kwenye mdomo wa juu, ukawa unaongezeka kila siku na mpaka ukafikia hatua hii (akinyoosha kidole kuelekeza mdomoni) niliyonayo sasa.
“Sikujua kama ningekuja kuwa nilivyo leo, naonekana kama kituko kwa watu kwa sababu wapo wananiogopa sana.”
KUGUNDULIKA KWA TATIZO
“Nilizunguka sana hospitalini wakati nikawa Ukerewe, Mwanza lakini sikupata matibabu yoyote huko kote nilikuwa nikiambiwa tatizo halionekani.
“Nikaenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza majibu yakawa yaleyale nao wakaniambia nije hapa Dar katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nilikuja moja kwa moja hapa nikafikia Magomeni Mapipa ndipo nikaanza rasmi matibabu kwa kufanyiwa kwanza vipimo mbalimbali.
“Baadaye nikaambiwa huu uvimbe nilionao umejaa damu na kama watanifanyia upasuaji uwezekano wa kupoteza maisha ni mkubwa na ili nipone natakiwa kwenda kutibiwa India, nililia sana.
AHADI ZA MUHIMBILI
“Mara ya mwisho nikiwa Muhimbili niliambiwa nitapigiwa simu ya kunitaka nijiandae na safari ya kwenda India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji, naona kimya kinazidi maana tangu nilipokwenda hospitali mara ya mwisho ilikuwa Mei, mwaka huu.”
Paulina aliongeza kuwa imebidi awe ombaomba ili apate angalau pesa ya kujikimu kwa sababu bado anasubiri matibabu.
“Tangu nilipokuja huku nina muda mrefu sijarudi nyumbani na niliwaacha watoto na baba yao, lakini kuna muda naikumbuka sana familia yangu ila nalazimika kuwa na subira kwani Muhimbuili wataalamu waliniambia nisubiri watu waliokwenda India wakirudi ndipo na mimi nitapigiwa simu.
ANAOMBA MSAADA
Mama huyo aliendelea kusema kuwa maisha yake anategemea kilimo na hakuwahi kwenda shule kutokana na hali ngumu ya maisha.
“Nateseka sana na huu ugonjwa, mdomo unaniuma mpaka nafikia hatua ya kushindwa kula na dawa yangu kubwa ni panadol kwa ajili ya kutuliza maumivu tu.
“Nawaombeni mnisaidie Watanzania wenzangu nateseka, kwa miaka nane kuugua siyo mchezo, mbaya zaidi sina msaada wowote.
“Nimevumilia lakini naona nazidi kuumia bila kupata tiba, ni bora ningerudi kwetu kama kufa nikafie huko kuliko kuendelea kuteseka huku ugenini,” alisema mama huyo, kisha akanyamaza na kuanza kufuta machozi kwa kutumia kanga yake.
0 comments:
Post a Comment