KWANZA napenda nianze kwa pongezi kwani kufanikisha tamasha la utoaji wa Tuzo za TAFA haikuwa ni shughuli ndogo, sote tunaweza kuongea kukosoa lakini TAFF wamefanya na tumeona ndio maana leo tunapata hata Kiburi cha kukosoa kwa sababu kinaonekana, hii haipotezi maana kuwa sisi hatuna mapenzi mema na waandaaji.
Ahadi ni Deni mimi na wewe tunadaiwa kwa wale waliotupa dhamana na kutuamini kama yale tuliyowaahidi tutayatekeleza kwao bila kutumia mamlaka vibaya kwa sababu wao wapo nje nasi ndani na kuwa wa kwanza kufika au kuongea na mtu wa mwisho, usiku nilipotoka katika tuzo za (TAFA)Tanzania Film Awards niliweka Deni.
Deni lenyewe niliahidi kufanya uchambuzi wa kina kuhusu mwenendo wa Tuzo hizo bila kumbeba mtu wala kumuonea mtu yoyote kwani naamini tuzo zile japo waandaaji ni TAFF lakini ni zetu sote kwani dhamana ya filamu tumewapa wao ikiwa ni kiungo kati yetu na Serikali.
Jumamosi iliyopita ilikuwa ni siku ya kuandikwa historia, sekta ya filamu nchini ikishuhudia utoaji wa Tuzo za Filamu (Tanzania Film Awards – TAFA), lakini tofauti na wengi walivyotarajia, tuzo hizi badala ya kuwahamasisha wasanii na wadau wa filamu zimewakatisha tamaa na kutugawa vipande pande.
Wengi wamekata tamaa kwa kuwa walitegemea tuzo zinazoandaliwa na chombo cha wasanii wenyewe (TAFF) zingekuwa na tija, wakiamini TAFF ipo kwa ajili ya kutetea na kupigania maslahi yao, kuhamasisha na kujenga weledi kama njia mojawapo katika kuimarisha ajira.
Hali ya tasnia ya filamu nchini kwa sasa inakatisha tamaa, viongozi wetu nahisi wamefikia ukomo wa kufikiri, wanaonekana kuridhika na hali ilivyo au pengine wamekata tamaa huku chombo wanachokiongoza kikikosa dira.
Wameshindwa kuifanya sekta ya filamu kuthaminiwa, imefikia hatua mtu mwenye busara hawezi kushughulika kabisa na filamu zetu. Kile tulichokuwa tukiaminishwa hakionekani tena, hakuna tena mipango ya kupasua mawimbi kwenda mbali zaidi. Kinachosubiriwa sasa ni kushuka badala ya kupanda!
Nathubutu kusema tasnia ya filamu ipo ICU (chumba cha wagonjwa mahututi) na inaelekea kufa kibudu kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa, Shirikisho halina dira wala viongozi waliopo hawana maono, hali ni mbaya sana, licha ya kuwa ndiyo fani inayoongoza kwa kutoa ajira kwa vijana wengi zaidi nchini.
0 comments:
Post a Comment